Na Jackson Kimambo
14th September 2010
Kuna umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu katika mazingira ya kazi ili kudumisha ufanisi hasa katika sekta binafsi na zile za umma ambapo waajiri na waajiriwa wanahitajika kupata elimu ya haki za binadamu mahali pa kazi kwa sababu kuna faida kubwa.
Michael Mushi, Meneja wa Meneja Mradi wa Haki za Binadamu Kazini wa shirika la Envirocare linalojishughulisha na utunzaji wa mazingira, jinsia na haki za binadamu alisema wameanza kutoa mafunzo ya umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu katika maeneo ya kazi kwa mashirika binafsi na yale ya umma.
Aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo na ufuatiliaji, uzingatiwaji wa haki za binadamu katika Kiwanda cha nguo cha 21st Century mjini Morogoro.
Anasema nchini Tanzania, watu wengi wanaofanya kazi kwenye maeneo mbali mbali hawajui haki zao na sheria zinazoilinda
Mushi akigusia faida za haki za binadamu kuwa ni pamoja na kuepuka vitendo mbali mbali vinavyoweza kuvunja haki za binadamu katika maeneo ya kazi.
Kila upande kwa maana ya mwajiri na mwajiriwa, alisema kuwa ni muhimu sana ukafanya wajibu wake ndipo dhana ya haki za binadamu katika maeneo ya kazi itakuwa na maana hata kuboresha utendaji kazi za siku kwa siku.
Kwa kutumia vipindi vya redio, Envirocare itaelimisha umma ili kupata uelewa na umuhimu wa haki za binadamu katika maeneo ya kazi.
Katika mafunzo hayo yaliyowashirikisha wawakilishi wa utawala wa viwanda na wafanyakazi wengine wa kawaida wakiwemo wasimamizi wa vitengo mbali mbali vya uzalishaji kiwandani hapo, Mushi alisema lengo ni kuboresha ufanisi.
Shiorika hilo Mushi alisema kuwa linajihusisha na utunzaji wa mazingira, Utetezi wa Haki za Binadamu na usawa wa Jinsia ili kuinua maisha ya wananchi hasa wale wa vijijini kwa kupitia kazi mbalimbali za kijamii.
Kama hiyo haitoshi, shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa jamii kuhusiana na haki ya mwanamke katika kumiliki na kurithi ardhi, haki za binadamu, usawa wa jinsia, mazingira na athari za viwatilifu katika mazingira.
“shirika lina wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali zikiwemo Kilimo, Sheria, Rasilimali watu, Jinsia, maendeleo ya jamii pamoja na mazingira,” anasema Mushi
Shirika limekuwa likiendesha miradi yake katika mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Pwani, Tanga, Mara, Iringa na Morogoro kwa kuhamasisha haki za binadamu katika mazingira ya kazi.
Kuhusu Haki za binadamu zimeundwa vizuri sana kisiasa na kielimu kwa kuzingatia viwango vinavyotokana na mikataba, makubaliano, maamuzi ya kisheria katika anga za kimataifa pamoja na taarifa za Umoja wa mataifa.
“ Maana ya haki za binadamu ni stahili ambazo mwanadamu yeyote anakuwa nazo na anapaswa kuzipata kwa sababu tu amezaliwa hai.Haki hizi zinajumuisha kuishi, haki ya kulindwa, haki ya usawa, haki ya kumiliki mali pamoja na haki ya kufanya kazi na kupata ujira stahiki ambayo ndio msingi wa maisha na kipimo cha utu” alisema.
Nchini Tanzania, haki za msingi za binadamu zimeainishwa katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inafanyiwa marekebisho mara kwa mara katika ibara ya 13 mpaka ya 16.
Kuhusu haki ya kufanya kazi ni ya msingi kwa binadamu ambayo imeainishwa katika katiba ni haki ya msingi ya binadamu ambayo haiwezi kuondolewa na mtu mwingine awaye yeyote.
Meneja huyo anasema kuwa, haki za binadamu katika maeneo ya kazi ni ibuko jipya katika kipindi hiki cha utandawazi kinachokabiliwa na uhaba mkubwa wa ajira, kote ulimwenguni mashirika ya haki za binadamu ikiwepo mashirika mbali mbali ya umoja wa mataifa yameweka vigezo vya kuzingatiwa katika maeneo ya kazi ili kulinda na kutunza haki za binadamu.
Mushi anasema kuwa mtu anayestahili kupata haki hizo ni binadamu yeyote anayefanya kazi halali katika maeneo mbali mbali ya uzalishaji wa bidhaa au huduma anastahili haki zilizoainishwa kwenye katiba kama sheria mama, ambazo ni lazima zizingatie viwango vya kimataifa na matamko mbali mbali ya umoja wa mataifa ya haki za binadamu.
Akielezea chimbuko la haki za binadamu katika maeneo ya kazi , Mushi anasema haki za binadamu katika maeneo ya kazi ni ukosefu wa ajira kwa nchi zilizoendelea, kwa sababu hiyo basi haki nyingi za binadamu zikawa hazizingatiwi katika sehemu mbali mbali za ulimwengu.
”Ili kulinda na kutetea haki za binadamu jamii ya kimataifa ikaunda tathmini ya utekelezaji wa haki za binadamu mbinu iliyoandaliwa kuweza kuvumbua na kusaidia kampuni kuona kama kuna ukiukwaji wa haki za Binadamu kwa wafanyakazi, wakazi na wadau unaotokana na matokeo ya utekelezaji wa kazi za kampuni,”anasema Mushi
Nchini Tanzania dhana hii ya haki za binadamu katika maeneo ya kazi inafadhiliwa na Shirika la Aim for Human Rights la Uholanzi chini ya uratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC).
Envirocare,limefanya tathmini kwenye sekta mbali mbali za uzalishaji wa bidhaa na huduma, ikiwemo viwandani na kugundua kwamba, sekta nyingi za uzalishaji hazijaweza kuzingatia haki za binadamu kwa ukamilifu pengine kwa kutokujua au kwa kutokujali.
Mushi anasema kuwa viwango na viashiria huboreshwa kila mwaka kwa kuzingatia mrejesho toka kwa wateja wa kampuni na wanaharakati wa haki za Binadamu, ili kuhakikisha kuwa, zana hii inashughulikia matatizo halisi ya maisha yanayozikabili kampuni pamoja na mabadiliko/maendeleo katika sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Meneja huyo alisema kuwa Envirocare inahusika kuangalia na kutathmini ni kwa kiwango gani haki za binadamu zinazingatiwa katika maeneo ya kazi.
Mushi anasema ili kulinda Haki za Binadamu katika mazingira ya kazi, Kampuni lazima iweke mipaka stahiki ya saa za kufanya kazi ili kutoa muda wa kutosha wa kupumzika na kustarehe.
Kulingana na viwango vya Mkataba wa shirika la kazi duniani, saa za kazi kwa wiki lazima yaishie saa 48 kwa pande zote za kibiashara na kazi za viwandani, lakini muda wa saa za kazi kwa siku katika viwanda vya kibiashara ni 10 na idadi ya saa kwa siku katika kazi za viwandani ni saa 8 (Shirika la kazi duniani linapendekeza kuwa serikali za Kitaifa zijielekeze kwenye saa 40 kwa wiki)
Mipaka ya saa za kazi ya Shirika la Kazi ni ( saa 8 au 10 kwa siku ) na yanaweza tu kuzidi katika mazingira mengine tofauti. Serikali zinawajibika kuandaa punguzo la saa hadi 48 kwa wiki, kwa mtu aliyeajiriwa katika nafasi za kiutawala au sehemu za muhimu.
Kufanya kazi kwa saa za ziada lazima kuwe kwa hiari na yasizidi saa 12 kwa wiki. Kama sheria ya nchi imeweka ukomo wa saa ya kazi kwa wiki hadi saa pungufu ya 48, saa za ziada zitaendelea 12 kwa wiki.
Pia kufanya kazi masaa ya ziada isiwe ni kitu cha kila siku. Hii inamaanisha kuwa, kampuni inaweza tu kuongeza idadi ya saa kutokana na mahitaji ya kipekee na yasiyotarajiwa ya soko. Ujira wa saa za ziada utalipwa kwa viwango au kama zawadi au bonasi.
Shirika la kazi duniani pia linatoa mapumziko ya wiki yasiyopungua saa 24 mfululizo katika kila kipindi cha siku saba za kazi.
Kampuni izingatie sheria za nchi katika kutambua kama punguzo au sheria za nchi ambamo kampuni inafanya kazi vinatoa muda zaidi masaa 48 kwa wiki na siku za kupumzika zilizowekwa na shirika la kazi duniani.
Shirika la kazi duniani halitoi viwango vya jumla kwa idadi ya mapumziko ambayo mfanyakazi anastahili kuwa navyo wakati wa kazi kwa siku.
Hata hivyo, kama nchi ambayo kampuni inafanya kazi haifafanui namba ya muda wa kupumzika, inapendekeza kuwa wafanyakazi waruhusiwe nusu saa ya mapumziko katika kila saa nne, kwa ajili ya kula, kujinyoosha na kupumzika.
Kama kazi inahitaji nguvu nyingi au ni ya kujirudia rudia, ni vyema wafanyakazi wapewe mapumziko mara kwa mara, hasa pale inapokuwa muhimu kuzuia uchovu au maumivu yanayotokana na ugumu wa kazi.
Hata hivyo ifahamike kwamba haki za mfanya kazi siyo tu kufanya kazi bali kuwa na mkataba wa kazi, ufafanuzi wa kazi, likizo, kulipwa saa za nyongeza,pamoja na faida mbali mbali zinazoambatana na mkataba wa kazi kama vile mafao ya uzeeni, bima ya afya kwa kuzingatia viwango vya kimataifa au kitaifa.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni
Kuwa wa kwanza kutoa maoni
No comments:
Post a Comment