Na John Ngunge
Suala la ubakaji kufanyika ndani ya ndoa kwa wanando au la, limekuwa linavuta hisia na kupewa mitazamo tofauti na watu tofauti. Makala hii yazungumzia baadhi watu mkoani Arusha wanavyolitazama suala hilo
Rehema Charles John (38) mke na mama wa watoto wawili na mkazi wa Sombetini, katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, anapata kigugumizi kusema bayana iwapo katika ndoa vitendo vya ubakaji vipo.
Mwanzoni anakubali kwamba , ubakaji ndani ya ndoa upo akitoa tafsiri sahihi ya jinsi anavyoelewa ubakaji, kwamba ni kitendo cha mwanamume kumwingilia mwanamke kimapenzi pasipo mwanamume huyo kupata ridhaa yake.
Kwa msingi huo, Rehema anajenga hoja kwamba, hata katika ndoa baadhi ya wanaume wamekuwa wakijikuta wakitumbukia katika jinai hiyo, pale wanapotumia nguvu na hivyo kuwalazimisha wake zao kufanya tendo la ndoa.
“ Ninachojua ubakaji ndani ya ndoa unatokea hasa kwa mwanamume anapotumia nguvu kufanya mapenzi na mkewe, ambaye kwa wakati huo hajisikii kufanya kitendo kama hicho, anaweza akawa amechoka au ana matatizo mengine…hivyo, akikataa na mume kulazimisha hapo ndipo mume anapofanya ubakaji,” anaeleza Rehema ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Kilombero mjini hapa.
Anasema vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa vinatokea hasa, wakati mume anapokuwa amekunywa pombe hali inayomfanya kutoelewa cho chote pale anapokataliwa au anapoelewa na mkewe kwamba hayuko tayari kufanya tendo hilo kwa wakati huo.
“ Hasa mume akiwa amekunywa pombe anakuwa haangalii na wala hasikii kukuru kakara zinazotokana na yeye kulazimisha. Mara nyingine mke ambaye hataki kupata aibu mbele ya watoto wake kutokana na kelele hizo anakubali yaishe ili kulinda heshima,” anaeleza.
Anasema hakuna mke ambaye anakusudia kumtesa mumewe lakini kama hajisikii kwa siku hiyo atakuwa anabakwa.
“ Ili kuogopa aibu kwa watoto inabidi mke akubali tu hata kama awali alikataa, inabidi afanye tu na mke anyamaze ili watoto wasijue baba na mama walikuwa wakifanya mambo hayo usiku,” anasema.
Hata hivyo, Rehema anaweka wazi kwamba, mambo kama hayo hayajamtokea yeye kwa kuwa, mumewe ni mtu mstaarabu na mwenye heshima katika ndoa yao.
Lakini kigugumizi cha Rehema kuhusu ubakaji ndani ya ndoa kinakuja pale alipoulizwa iwapo anaweza kumshtaki mumewe kwa kosa la kumbaka.
“ Nitaenda kumshtaki wapi, kwa wazazi wake au nitaenda kumshtaki mahakamani, ili iweje? Huyo ni mume wangu itakuwaje nimshtaki,” anahoji na kuongeza, “ kama kuna tatizo ni vema mwanamke akamweleza mwenzake ili avumilie hadi hapo tatizo litakapokwisha.”
Kigugumizi kama hicho alikipata pia John Paulo, baba wa watoto wawili na mkazi wa Moshono mjini hapa. Awali John, alizungumzia kukubali kwamba ndani ya ndoa kuna ubakaji, lakini baadaye alisema, hakuna mwanamume anayebaka mke wake.
Msingi wa kukubali kwake awali, ulitokana na tafsiri aliyoitoa kwamba, kitendo cha ubakaji ni kumwingilia mwanamke bila ridhaa yake hata kama kitendo hicho, kitakuwa kikifanywa na mume kwa mkewe.
“ Ubakaji ndani ya ndoa upo pale mmoja anapofanya kitendo hicho wakati mwingine amechoka au kama hataki kwa sababu fulani za msingi,” anasema.
Hata hivyo, anasema wapo wake wengine ambao kutokana na ujeuri wao, wanatumia hiyo kama silaha ya kuwakomoa waume zao, na hapo ndipo John anapohoji, “sasa mume anapokataliwa na mkewe aende wapi.”
Anasema katika hali hiyo, inabidi mume atumie nguvu ili kupata haki yake, lakini anasema likifanyika wakati wa maelewano linakuwa zuri.
Sheria Maalum ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998, (SOSPA) inaeleza ubakaji kama kitendo cha mwanamume kumwingilia mwanamke ukeni, kwa nguvu pasipo ridhaa yake kwa lengo la kutaka au kufanya naye mapenzi.
Inataja kuwa, kufanya kitendo hicho ni kosa la jinai ambalo mtuhumiwa akitiwa hatiani anaweza kupata adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au maisha.
Lakini wakati suala hilo likiwa hivyo, hivi karibuni, washiriki wa mafunzo yanayotolewa na shirika la Hakikazi Catalyst la mkoani Arusha kwa wanaharakati, maafisa watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji wapatao 80 kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara walizua mjadala mzito wakati mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Rehema Mwateba, alipokuwa akitoa mada yake kuhusu somo la jinsia.
Katika somo hilo, Rehema ambaye ni mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya kijinsia nchini, alielezea istilahi zinazohusiana na maumbile, kazi za jinsi, jinsia, malazi, mahitaji maalum ya kijinsia na mambo kadha wa kadha, pia alizungumzia suala la kubakwa, kubaka na ubakaji.
Rehema alifafanua kwamba, kubakwa ni kitendo cha mwanamke kuingiliwa ukeni bila ridhaa yake, wakati kubaka ni kumwingilia mwanamke wa umri uwao wo wote ule, kwenye uke wake bila ridhaa yake na ubakaji ni kitendo cha kumwingilia mwanamke ukeni bila ridhaa yake.
Baada ya tafsiri hizo, ndipo mjadala ulipozuka kuhusu ubakaji ndani ya ndoa, ambapo vuta ni kuvute ilizuka kati ya wanaume na wanawake.
Wanaume walikuwa wakisisitiza hakuna ubakaji ndani ya ndoa, wakati wanawake kwa upande wao walisema wengi wao wanabakwa na waume zao.
Wanaume waliokuwa wakipinga, walienda mbali zaidi na kuitaka serikali kuifanyia marekebishao sheria ya SOSPA, ili tafsiri isemayo ubakaji ni kumwingilia kimwili mwanamke bila ridhaa yake isiwahusu watu wenye ndoa.
Wakijenga hoja walisema, wakati wa kufunga ndoa tayari mwanamke anakuwa amekwisharidhia kuwa mke, na kwa sababu hiyo hakuna haja ya kuridhia mara kwa mara kila wanapohitaji kufanya tendo hilo.
Mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies of God la Tengeru, mkoani Arusha, Vumilia Samuel Isanje, alisema hakuna ubakaji kwa watu wenye ndoa.
“ Ubakaji kwenye ndoa uondolewe…ni vizuri mwanamke akaelewa kwamba muda wo wote jambo hilo linaweza kutokea, na anakuwa amekwisharidhia tangu walipofunga ndoa kufanya tendo hilo na mumewe, hivyo hakuna haja ya kuridhia mara kwa mara wanapohitaji kufanya hivyo.
Kwa upande wake, Ezekiel Muhubiri kutoka asasi ya Kiungo ya mkoani Kilimanjaro, alisema alishauri kuwekewa mipaka kwa sheria ya SOSPA.
“Sheria hii iwekewe mipaka, hili ni suala la kuandaana, sheria ifanyiwe marekebisho kwani huko sio kubaka, bali mwanamke anakuwa hajaandaliwa, lakini kama inakuwa kwa mwanamke wa nje basi hapo panahitajika ridhaa yake,” alisema.
Lakini wanawake kwa upande wao, walikuwa wakisisitiza kwamba ndani ya maisha ya ndoa ubakaji upo.
Walikuwa wakifafanua kwamba ubakaji katika ndoa unakuja pale mwanamume anapohitaji kupewa haki yake ya ndoa, lakini kwa bahati mbaya mwezi wake anakuwa hayupo tayari pengine kwa sababu za kiafya au kuchoka.
“Ubakaji ndani ya ndoa upo, pale mwanamke anapokuwa hajisikii kwa tendo hilo lakini mwanamume analazimisha…hapo anabaka, mwanamke anakuwa hayupo tayari kwa tendo hilo,” alisema mwanamke mmoja.
Alisema kwa ujumla tendo hilo ni la maelewano lakini katika mazingira fulani wanaume wanakuwa wakilazimisha kufanya tendo hilo na hapo ndipo ubakaji unapoingia.
Mshiriki mwingine kutoka kijiji cha Eworendeke, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, Nengolong Sadala, alisema suala la ngono ni la maelewano kati ya mume na mke na inapotokea mmoja anatatizo fulani mwingine anatakiwa kuwa na uvumilivu.
Akiunga mkono kauli hiyo, mkazi mwingine wa kijiji hicho, Noorkimunyak Ndoori, alisema anasikia kuwa wapo baadhi ya wanaume ambao wanalazimisha kwa nguvu kupewa unyumba kwa wake zao wakati sual hilo ni la maelewano.
“ Unamkuta mwanamke ni mgonjwa au wakati mwingine amechoka, lakini mwanaume analazimisha apewe haki yake, kufanya hivyo ni sawa na kubaka,” alisema na kuongeza, “kinachohitajika hapa ni maelewano na mmoja kumwandaa mwenzake na sio kulazimisha.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment