KARIBUNI MCHICHANI

Kwa Habari moto moto Kuhusu Siasa , Uchumi, Maisha, Elimu Na Mengine Mengi.



Tuesday, September 14, 2010

Mtanzania anayefuata nyayo za Oprah Winfrey

Tumezoea kuwaona watangazaji na waendesha vipindi vya televisheni maarufu kama vile Oprah Winfrey na kipindi chake Oprah Winfrey Show na Tyra Banks na kipindi chake The Tyra Banks Show wote hawa wakiwa ni wanawake wa Kiafrika wenye asili ya Marekani waliofanikiwa na kujizolea umaarufu kutokana na vipindi vyao hivyo.
Pamoja na kuwa ni Wamarekani weusi, lakini bado tukiwa kama Watanzania hatuwezi kujitapa ama kujivunia sana pamoja kwamba kwa asili wana damu ya Kiafrika.




Lakini sasa huenda umefika wakati wetu nasi kujivunia watu wetu, watangazaji wetu, Watanzania wenzetu ambao wameamua kuvunja ukuta na kujitosa katika uendeshaji wa vipindi ama maonesho ya televisheni kama ilivyo kwa Oprah na Tyra.



Tuna kila sababu sasa kama watanzania kujivunia kwa sababu tumepata Mtanzania mwenzetu ambaye ameamua kuendesha kipindi cha mazungumzo katika televisheni, na huyu si mwingine bali ni Irene Sporah Njau ambaye ameanzisha Kipindi cha Majadiliano cha Kiafrika kinachojulikana kama The Sporah Show akiwa nchini Uingereza.



Kama hiyo haitoshi, binti huyo kutoka Tanzania ambaye hujulikana zaidi kwa jina la Sporah kuanzia Juni 11 The Sporah Show itakuwa ikioneshwa hapa nyumbani kupitia kituo kimojawapo cha televisheni nchini katika siku za Ijumaa na Jumamosi.



Sporah na kutaka kufahamu kwa undani kuhusiana na mwanadada huyu, kazi zake, vipindi vyake na urushaji wa vipindi vyake hapa nyumbani Tanzania. Yafuatayo ni mahojiano kati yetu na Sporah anayerusha kipindi chake kupitia kituo cha televisheni cha BEN cha Uingereza;



Kwa Jina ni Irene Sporah Njau. Kuhusu elimu yangu, naweza kusema katika purukushani za kutafuta maisha nilijikuta nasomea vitu tofauti.
Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Biashara za Kimataifa, nina Stashahada ya Uhasibu na Utawala wa Biashara, nina Stashahada ya Utangazaji wa Televisheni, na nina Cheti cha Teknolojia ya Habari.




Akielezea historia yake Sporah alikuwa na haya ya kusema



Mimi ni mtoto wa mwisho katika familia yangu, nilimaliza Kidato cha Sita Kampala, Uganda na baada ya hapo nilikuja nchini Uingereza kujiendeleza na masomo.



Kwa kweli TV Show ilikuwa ni ndoto yangu, ila nilipofika Uingereza na kuona jinsi ambavyo nchi za wenzetu zina mifumo tofauti ya kuelimisha jamii, nilijikuta vikinipa motisha zaidi ya kutaka kutimiza ndoto yangu ndipo nilipopata wazo la kuanzisha kipindi cha The Sporah Show.



Ukizingatia kwamba hakukuwa na kipindi kingine cha televisheni kilichokuwa na dhamira kama yangu ya kuelimisha, kuburudisha na kufahamisha, hasa katika jamii yetu ya watu wa kutoka nchi za Kiafrika hapa Uingereza na Ulaya.



Mimi na timu yangu tukiwa kama waanzilishi wa African Talk Show hapa Uingereza na Ulaya kwa ujumla, napenda kumshukuru Mungu mwitikio ulikuwa mzuri sana nilipoanzisha kipindi changu na hivyo inanipa morali zaidi ya kufanya kazi kwa juhudi.



Ukiwa Mtanzania unayeishi nje ya nchi, tungependa kufahamu unaonaje utofauti wa maisha nyumbani Tanzania na nje unakoishi.



Kwa kweli tofauti ipo, lakini sio kubwa sana, naweza kusema tofauti kubwa ipo kwenye utamaduni na maadili.



Lakini vitu kama vyakula, jinsi ya kuishi na watu, jinsi ya kuzungumza na watu, hivi ni vitu ambavyo vina tofauti kubwa sana na nchi za Ulaya na vinakua changamoto kubwa zaidi hasa pale ukiwa kwenye mambo ya kibiashara na watu wa nchi zingine.



Je, ulisomea masuala ya uandishi wa habari au ulisomea taaluma gani nyingine?



Its really funny kwa sababu wakati naanza mambo ya TV Show nilikuwa nasomea mambo ya uhasibu.



Lakini nilipoona watu wananikubali nikaamua kwenda kuchukua kozi ya Utangazaji wa Televisheni ili kujua mambo muhimu yanayotakiwa katika sekta hii ya habari, hivyo nina Stashahada ya Utangazaji wa Televisheni. Kwa hiyo sijasomea uandishi wa habari.



Ni lini ulianza kutengeneza vipindi vyako na kurusha, na nani alikuhamasisha au ulivutiwa na nani hadi ukatamani nawe uwe na kipindi cha televisheni.



Nilianza kazi ya Utangazaji wa Televisheni mwaka 2006, wakati huo nilikuwa nafanyia watu mahojiano ya ana kwa ana (One to One). Lakini mwaka wa 2007 ndio kipindi cha The Sporah Show kilianza rasmi.



Mimi ni mpenzi wa TV Show tangu nikiwa mdogo, ila nilivutiwa zaidi na nilivyofika Ulaya na kuona jinsi TV Show zinavyofikisha ujumbe kiurahisi na kwa watu wa aina zote bila kuchagua rika, rangi wala dini.



Nilifanya utafiti wangu nikagundua kuwa hapa Uingereza na Ulaya kwa ujumla hakuna TV Show ambayo ilikuwa inalenga jamii ya Kiafrika haswa katika masuala ya kuelimisha, kufahamisha na kuburudisha, ndipo nilipoona nichukue nafasi hii kufanya kitu ambacho nilikuwa nikiota kwa muda mrefu, na huo ndio ulikuwa mwanzo wa kipindi changu cha The Sporah Show.



Chimbuko la kuendesha vipindi vya televisheni ilikuwa ni nini?



Televisheni ni njia pekee na rahisi ya mawasiliano, dhamira yangu ilikuwa ni kuwakutanisha watu wa rika na nyenzo tofauti kukaa pamoja na kuongea mambo mbalimbali yanayohusu jamii kwa ujumla kama kuelimishana, kuhamasishana, kuburudisha, kurekebishana na mengineyo mengi, hii yote ni kusaidiana katika maisha yetu ya kila siku na kujifunza mambo mapya.



Ikiwa ni Mtanzania wakati unaanza kurusha vipindi vyako hukupata changamoto zozote, maana watu wengine huona kama Waafrika hawawezi kufanya mambo mazuri?



Swali zuri sana, Asante. Kwa kweli changamoto zilikuwepo na bado zipo na ninaamini zitazidi kuwepo tu hasa kwa sababu The Industry is growing (maana yake sekta hii inakua).



Ila changamoto ambayo ilikuwa inakatisha tamaa ni Language Barrier (kizuizi katika lugha), na pale watu wanapokuwa wanakufananisha na watu wakubwa kama kina Oprah Winfrey.



Tatizo sio kama Waafrika hatuwezi kufanya mambo mazuri, Hapana! Naamini kabisa Waafrika tunaweza kufanya kitu chochote kile ambacho watu wa mataifa mengine wanafanya ilimradi tu uwe na juhudi.



Tatizo ni kwamba Waafrika wengi pale wanapokuwa wanafanya kitu haswa nchi za Ulaya wanakuwa wanafananishwa na watu wenye uzoefu wa hali ya juu, hii inakatisha tamaa sana na hapo ndipo wengi wanakata tamaa ya kujaribu kufanya vitu vizuri.



Je, huwa unafuatilia vipindi vya televisheni hapa Tanzania?



Ndio, nafuatilia sana televisheni za Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwa sababu moja ya madhumuni ya The Sporah Show ni kurushwa katika nchi zote za Afrika na dunia nzima kwa ujumla.



Ni mtangazaji gani au mtu gani anayekuvutia katika sekta ya habari hapa nchini Tanzania na nje ya nchi.



Kwa kweli nina watangazaji wengi wanaonivutia kutoka Tanzania, na mmojawapo ni Suzan Mungy.



Nilikutana na Suzan katika Tanzania Diaspora UK 2010, She is an amazing person. Hapa Uingereza navutiwa sana na Trisha Goddard ambaye ni mtangazaji mzuri sana na bila kumsahau Malkia wa Talk Show Oprah Winfrey, She is remarkable.



Lengo lako ni kufika wapi kisekta?



Sporah: Lengo langu ni kuendeleza kipindi cha The Sporah Show kiweze kurushwa katika nchi zote za Kiafrika na ulimwengu mzima kwa ujumla.



Vipindi vyako hasa vinaangalia masuala gani au umewalenga watu wa namna gani?



Vipindi vya The Sporah Show vinaongelea mambo mengi tofauti yanayohusu jamii kwa ujumla kinaelimisha, kinafahamisha na pia kuburudisha. Naweza kusema tumewalenga watu wa rika tofauti hasa kizazi kipya.



Nani mwingine katika familia yako anapenda masuala ya televisheni au masuala ya habari?

Sporah: Its surprising (inashangaza) hakuna hata mmoja.



Mbali na vipindi vyako kurushwa Tanzania una mpango wa kupeleka katika nchi nyingine za Afrika?.



Sporah: Ndio haswa, tunafanya kazi kwa juhudi zote ili kipindi cha The Sporah Show kiweze kurushwa katika nchi zote za Afrika na dunia nzima kunapo majaliwa.



Vipindi vitakavyokuwa vikionekana katika televisheni ya Tanzania utakuwa unavifanyaje au vitapatikana kwa utaratibu gani?



Vipindi vitakavyokuwa vinarushwa havitakuwa na tofauti kubwa sana na vya nchi nyingine ila naweza kusema; mtu kwao, kwa hiyo tutakuwa tunachanganya Kiswahili na Kiingereza, niseme tu The Sporah Show itakuwa ikirushwa kwa watazamaji wa Tanzania itakuwa ni KISWA-NGLISH.



Ulipata wapi mtaji wa kuanzisha kipindi au uliwezaje kuanzisha kipindi hiki?



Sporah: Kabla sijaanza The Sporah Show nilikuwa nafanya biashara ya kuuza nywele za akina dada kwa njia ya mtandao (Online) na nguo za asili (Batiki na viatu vya Kimasai).



Hapo ndipo nilipojikusanya kusanya na kuanzisha na kupata fedha nikaanzisha Kampuni ya The Sporah Media Production.



Labda tangu ulipoanza ni mahojiano gani ulifanya na yataendelea kubaki katika kumbukumbu zako?



Sporah: Kusema kweli kila mahojiano ninayofanya yanakuwa na kitu chake tofauti cha kukufanya ukumbuke baadaye, hii ikiwa ni mojawapo.



Unawaambia nini vijana wenzako na wanawake, au ushauri gani unawapa katika kufanikiwa.

Kwa vijana wenzangu, ningewashauri kuwa makini na shule, maana dunia tunayoenda haina upendeleo, ila ni elimu yako ndio itakayoongea, na pia kujitahidi kufanya kazi kwa juhudi bila kuchagua kazi. Hivyo mafanikio yatakuwepo tu.




Lakini pia angalia marafiki,vijana wanatakiwa kujaribu kuepukana na makundi ya marafiki ambao sio wazuri, kwa sababu vijana wengi wanapotoka kwa sababu ya makundi ya marafiki.



Labda “rafiki yangu anakunywa pombe nami nakunywa, mwingine ana boyfriend na mimi nataka ku na boyfriend� na mengineo mengi. Hili ni tatizo kubwa linalopotosha vijana wengi wa kizazi cha sasa.



Anaendelea kusema: Kwa wanawake wenzangu, ningependa kusema shule ni muhimu sana kwa mtoto wa kike kwa sababu itakupa nguvu ya kujiamini katika mambo mengi unayoyafanya au mambo mengi utakayopitia katika maisha kama mwanamke. Ni vizuri wanawake kujua kwamba, chochote ambacho mwanamume anaweza kufanya, mwanamke anaweza kufanya, tena kwa ufasaha zaidi.



Unajua nini, inapendeza sana mwanamke akiwa anajiamini na kila kitu anachokifanya na sio kufuata mkumbo. Mimi nadhani cha muhimu sana for a women is to be YOURSELF so you will be able to know WHO YOU ARE, and what you can do better and what you can not do.



Kwa kweli siri ya kufanikiwa ni kufanya kazi kwa bidii, kujua ni nini unaweza kukifanya kwa moyo wako wote na sio kwa sababu umemuona jirani au rafiki anafanya.



Ukifanya kitu unachokipenda inakuwa ni ngumu sana kukatishwa tamaa na pia ni rahisi sana kuongeza juhudi kwa vyovyote vile.

picha_4

Ni vitu gani unapendelea sana kufanya muda wako wa ziada au njia ya kujipumzisha na kazi zako?



Mimi ni muumini mzuri hivyo napenda kwanza kanisani na pia napenda kujifunza vitu vipya.



Huyo ndiye Irene Sporah Njau ambaye kipindi chake kinavutia takribani watazamaji 900,000 kote Ulaya na dunia nzima kupitia BEN televisheni, kituo kikubwa cha televisheni barani Ulaya kinachogusa kwa karibu zaidi mambo ya Waafrika

No comments:

Post a Comment