Miss Tanzania 2010, Genevieve Emmanuel (katikati)akipunga mkono, akiwa na mshindi wa tatu, Consolata Lucas (kushoto) na mshindi wa pili Gloria Mwanga baada ya matokeo kutangazwa. GENEVEIVE Emmanuel ambaye ni mtoto wa Meneja wa timu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam
inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Emmanuel Mpangala, ndiye Miss Tanzania mwaka 2010.
Mrembo huyo ambaye pia ni Miss Temeke 2010, sasa amelirudisha taji la Miss Tanzania jijini Dar es Salaam baada ya kuwa mkoani Mwanza kwa miaka miwili mfululizo.
Taji hilo lilikuwa linashikiliwa na Miriam Gerald ambaye alitwaa taji hilo mwaka jana akitokea mkoani Mwanza, akilirithi kutoka kwa Nasreem Karim ambaye alilitwaa mwaka 2008 na kumaliza utawala wa Dar es Salaam katika mashindano ya urembo hapa nchini.
Nasreem aliyekuwa mrembo wa Kanda ya Ziwa akitokea mkoani Mwanza, aliwabwaga warembo wenzake 27 waliokuwa wakiwania taji hilo.
Kwa miaka mingi taji la Miss Tanzania lilikuwa likichukuliwa na warembo kutoka kanda za Dar es Salaam, ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni, lakini tangu Nasreem amalize utawala huo taji hilo kwa miaka miwili sasa limehama Dar es Salaam.
Baada ya Saida Kessy aliyetwaa taji akitokea mkoani Arusha mwaka 1997, hakuna mrembo mwingine nje ya Dar es Salaam aliyetwaa taji hilo baada ya hapo.
Pia tangu mwaka 2004 Kanda ya Kinondoni nayo imekuwa ikitoa Miss Tanzania, hivyo ushindi wa mrembo huyo wa Mwanza ulifungua historia mpya katika mashindano hayo.
Warembo wengine waliopata kutwaa taji la Miss Tanzania tangu yaanze tena mwaka 1994 na miaka yao katika mabano ni Aina Maeda (1994), Emilly Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999) na Jacqueline Ntuyabaliwe (2000).
Pia wapo Happiness Magesse (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumary (2005), Wema Sepetu (2006) na Richa Adhia (2007).
Mrembo huyo anakuwa wa tatu kutoka Temeke kutwaa taji la Miss Tanzania, ambapo wengine walikuwa mwaka 2001 na 2004.
Akitangaza matokeo ya mashindano hayo juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Prashant Patel alitangaza Taji la Miss mwenye kipaji kuchukuliwa na Flora Florence ambaye ni Miss Morogoro, huku mrembo wa Utalii wa ndani akiibuka Salma Mwakalukwa ambaye alikuwa mshindi wa pili Miss Ilala.
Balozi wa Redd’s aliibuka Consolatha Lukosi. Miss Ilala 2010 Bahati Chando hakuingia kumi bora.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, mama mzazi wa Miss Tanzania, Maria Mpangala alisema ushindi wa mwanawe ni zawadi kwa familia yao na kwamba walimsaidia kwa kila hali kufikia hatua hiyo.
Kwa mujibu wa mama huyo, Geneveive alimaliza kidato cha sita mwaka huu katika sekondari ya Ruaha iliyopo Iringa na alikuwa akisomea masomo ya Historia, Jiografia na Lugha (HGL).
Katika shindano hilo, Miss Kanda ya Kati, Wilemi Etami aliteleza na kuanguka chini baada ya kumaliza hatua ya kujitambulisha.
Burudani mbalimbali zilisindikiza shindano hilo kutoka kwa wasanii wa kundi la THT pamoja na TMK Wanaume Family.
KUMI BORA MISS TANZANIA 2010
TANO BORA YA MISS TANZANIA 2010
Hatimaye Geneveive Emmanuel Miss Tanzania 2010
Miss Tanzania 2010 , safari njema katika kupeperusha bendera ya taifa Miss World
No comments:
Post a Comment