KARIBUNI MCHICHANI

Kwa Habari moto moto Kuhusu Siasa , Uchumi, Maisha, Elimu Na Mengine Mengi.



Sunday, September 19, 2010

TUNAJIFUNZA NINI KUTOKA KWA BOB MARLEY AU KULA DUDE LA KIMATAIFA !!!!!! ????

                   

Bob Marley



Mcheza mpira wa miguu, Mhubiri wa amani na upendo, Mwanamapinduzi, Mwanaharakati, Mpiganaji, Mwanasiasa, Mwanamuziki wa Reggae na Nyota ya kwanza katika ulimwengu wa tatu Bob Marley.




Alizaliwa akiitwa Robert Nesta Marley na mama wa Kijamaica mwenye asili ya Afrika, bi Cedella Booker na baba mwanajeshi Mwingereza aliyefariki kijana Robert akiwa bado mdogo sana akiwaacha katika umasikini mkubwa.



Bob Marley alizaliwa panapo usiku wa kuamkia Februari 6, 1945, St Anns Parish kijiji cha Nine Miles (maili tisa) huko Jamaica.



Kumbukumbu zake za utotoni na ujanani zimejaa harakati za maisha na muziki. Harakati zilizomkutanisha na kijana machachari Peter Tosh na pia Bunny Livingstone (Wailer) na hatimaye vijana wengine kama Junior Braithwaite na Beverly Kelso. Panapo mwaka 1963, Bob akiwa na wenzake waliojiita Wailing Wailers waliweza kusaini mkataba na prodyuza maarufu wakati huo Coxsone Dodd na kutoa vibao kadhaa kikiwemo 'Simmer Down' kilichowatambulisha vema katika ulimwengu wa muziki wa Jamaica.



Bob na Rita Anderson walioana mwaka 1966 baada ya Bob kurejea Jamaica akitokea Marekani ambako alikacha kwenda vitani Vietnam. Aliporudi Jamaica, Bob alikuta imani ya Kirastafari ikiwa imepamba moto kufuatia ziara ya Mfalme wa Ethiopia Haile Sellassie (Ras Tafarr Makonen) hapo mwaka 1965. Hotuba ya Sellassie ndicho kibao cha Bob kiitwacho 'War'



Kundi la Wailing Wailers halikudumu sana. Lilivunjika mwaka 1974 na Bob kuunda kundi lake maarufu zaidi katika historia ya muziki wa reggae la 'Bob Marley and the Wailers' wakafanikiwa kutoa albamu ya 'Catch A Fire' panapo mwaka 1975 ikiwa na kibao maarufu kilichopatwa kuimbwa tena na wanamuziki wengi sana cha 'No Woman No Cry'



Mwaka 1976, Bob Marley alifanikiwa kuwapatanisha mahasimu wakubwa wa kisiasa nchini Jamaica, waziri mkuu na kiongozi mkuu wa upinzani, Michael Manley na Edward Seaga. Wajamaica walimwona Bob Marley kama shujaa halisi wa taifa lao. Bob na kundi lake walishambuliwa na risasi siku tatu kabla ya tukio hilo, lakini walipona.



Mwaka huohuo wa 1976, Bob Marley na kundi lake walitoa albamu ya 'Exodus' iliyovunja rekond ya mauzo na kukaa kwenye chati ya Billboard kwa majuma 52 ikikamata namba moja.



Bob Marley alizunguka mabara yote ya ulimwengu kupiga muziki wake uliokubalika sana. Maonesho makubwa zaidi aliyafanya Uingereza, Ujerumani, New Zealand, St. Barbara, California huku pia akishiriki kama mgeni mwalikwa muhimu katika sherehe ya uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980.



Maradhi ya kansa iliyoanzia kidoleni mguuni kwake, yaliukatisha uhai wake panapo Mei 11, 1981 huko Miami Marekani akiwa angali kijana wa umri wa miaka 36. Katika kibao chake cha 'Rastaman Chant' alipata kusema, "One bright morning when my work is over, I'll fly away to Zion"

Hata hivyo aliiacha kazi yake kama mhubiri wa amani na upendo.



Serikali ya Jamaica, kwa kuutambua mchango wake, ilimtunukia nishani ya juu zaidi 'Order of Merit.'



Bob Marley aliacha watoto 12, wengi wao wanajihusisha na muziki wa reggae na hip hop.



Bob Marley atakumbukwa zaidi duniani kama balozi na shujaa halisi wa muziki wa reggae. Atakumbukwa kwa kuuweka muziki huu wenye nguvu katika ramani ya ulimwengu.



Muziki wake utaendelea kuishi vizazi na vizazi. Ni urithi muhimu sana. Ama kwa hakika twajivunia sana miaka 36 ya uhai wake.



Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi daima. Amina.


 Tukiwa tunakumbuka miaka 29 ya kifo cha mwanamapinduzi Bob Marley, wacha tutafakari falsafa yake kidogo.

                                                                  
BOB MARLEY
Katika kibao cha JAH LIVE anasema...the truth is an offence. Sote tumeona, waliosema ukweli, wameitwa wanafiki na wazandiki. Lakini wacha tujipe nguvu na kibao chake cha SMALL AXE, maana alisema...we are small axe...you're big tree..we gonna cut u down. Ama kwa hakika shoka dogo huangusha mbuyu.


Katika BABYLON SYSTEM hakusita kusema...we refuse to be what you want us to be...we are what we are. Ndivyo, tutakuwa vile tulivyo. Maana alisema...you can't educate us...for no equal opportunity. Tutapambana ili usawa uwepo katika elimu.



Alipokuwa Zimbabwe, katika kibao chake ZIMBABWE hakusita kusema...every man got a right to decide his own destiny. Waama, tuna haki ya kujiamulia mustakabali wa maisha yetu. Mbele akasema...to divide and rule could term us apart. Nawakumbusha Watanzania na Waafrika tusimame kwa umoja ili tuwe imara.

  Tazama sasa katika WAR hakusita kusema...until there is no longer first class and second class citizens of any nation. Wale wanaoathiriwa na maji ya mgodini kule Tarime nao wanapaswa kujeshimiwa na kuthaminiwa. Bob akakumbusha....we are in confident of victory over evil. Chambilecho Bob, wema hushinda uovu.



Mtafakari katika REDEMPTION SONG maana alisema...emanicipate yourself from mental slavery...none but ourselves can free our minds. Tujikwamue kutokana na utumwa wa kiakili. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Tutumie vema akili zetu. Hakuna atakayetukomboa.


Katika GET UP STAND UP tukuwakumbushe 'hao' maneno ya Bob..you can fool some people sometime...but you can't fool all the people all the time. Wanatudanganya, lakini hawawezi kutudanganya wakati wote. Nasi tusimame na kupigania haki zetu.



                                                                       Hebu fikiria katika SURVIVAL alipowaambia watawala...how can u be sitting there...telling me that u care...when I look around the people suffer. Sote twaona ama kwa hakika maana halisi ya maneno haya.


Roberth Nesta Marle        
Nimalizie kwa busara yake katika JAMMIN' maana alisema...no bullet can stop us now...we neither beg nor we won't bow..neither can be bought nor sold...we all defend the right...Jah children must unite...for life is worth much more than gold. Ingawa kwetu hususani kule kwenye mgodi wa North Mara....dhahabu ina thamani kuliko maisha ya watu.

No comments:

Post a Comment