Wajumbe waangua kilio mkutanoni
Vidonda vya kura za maoni bado vinakiumiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Tarime na juzi kikao cha usuluhishi na kuvunja kambi kilichokuwa kimeitishwa kiilisha bila kufikiwa kwa azma hiyo, baada ya baadhi ya wajumbe kuanza kuangua kilio wakiongozwa na mgombea aliyeangushwa akiamini alishinda kura hizo.
Katika hali isiyo ya kawaida, mgombea huyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba mkoani Shinyanga, Christopher Kangoye, anadaiwa kuangua kilio, alipowekwa ‘kiti moto’ akitakiwa kulivunja kundi lake ndani ya CCM wilayani Tarime.
Hata hivyo Kangoye mwenyewe jana alikanusha kuangua kilio alipozungumza na NIPASHE kwa simu na kusema hizo ni habari za waandishi wa habari za kukuza mambo.“Hayo najua ni mambo ya waandishi wa habari,” alisema Kangoye.
Vyanzo vya habari ndani ya mkutano huo uliofanyika Jumamosi vilisema kwamba Kangoye ambaye alishindwa na Nyambari Nyangweni, alijikuta akifikwa na machungu hayo kutokana na kile anachoamini kuwa alipokwa ushindi kwa hila kwani ndiye alikuwa ameongoza kwa idadi ya kura za maoni, lakini kura zikachakachuliwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia NIPASHE, Kangoye aliitwa katika kikao cha kamati ya siasa ya CCM wilayani Tarime.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Rashid Bogomba na Kaimu Katibu wake, Felex Manyama.
Pia walikuwepo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa wilaya hiyo, Samwel Magabe na Ofisa Uchumi, John Gimunta.
Taarifa kutoka ndani ya CCM wilayani hapa zilieleza kuwa, Kangoye alibubujikwa machozi kiasi cha kuwafanya wafuasi wake takribani 40 walioalikwa katika kikao hicho, kutokwa machozi pia.
Kutokana na vilio hivyo, taarifa zinadai kuwa kikao hicho kiliahirishwa.
Taarifa hizo zilidai kuwa kikao hicho kiliitishwa mahususi kwa ajili ya kumtaka Kangoye atoe tamko la kuvunja kundi lake analodaiwa kulianzisha kwa takribani miaka 10 iliyopita. Kangoye ndiye aliyeshinda kura za maoni wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Zakayo Wangwe.
Hata hivyo Kangoye alishindwa na Charles Mwera aliyewania kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ingawa hivi sasa anagombea kupitia Chama Cha Wananchi (CUF).
Kundi la Kangoye linadaiwa kuiweka CCM katika wakati mgumu, hivyo kuwa kikwazo na kudhoofisha nguvu za chama hicho jimboni Tarime.
Ilielezwa kuwa baada ya Bogomba kufungua kikao hicho, wajumbe walitaka baadhi ya watu kutolewa nje kwa madai ya kukosa sifa za kuhudhuria.
Waliotakiwa kutolewa nje ni pamoja na Katibu Msaidizi, Adirian Moris, Ofisa Uchumi, John Gimunta na Maxmilian Matinde.
Wajumbe waliotolewa nje walidai kuwa, kikao hicho kisingekuwa halali kwani makundi ya pande mbili zinazotuhumiana yalistahili kuwepo.
Mmoja wao ambaye hata hivyo hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema kikao hicho kimechochea vurugu badala ya kuleta suluhu ndani ya CCM.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa, Bogomba alimpa nafasi Kangoye ili awaombe wafuasi wake kuvunja makundi na kujiunga na wenzao katika kampeni zinazoendelea.
Kangoye alikaririwa akisema: “Ndugu zangu nawaombeni mkipe kura Chama Cha Mapinduzi, ingawa tulionewa…” kisha alishindwa kuendelea na kuanza kububujikwa machozi.
Hali hiyo ilidaiwa kusababisha wafuasi wake kuangua kilio, hivyo kukifanya kikao hicho kuwa eneo la majonzi.
Vilio na machungu ya Kangoye na wafuasi wake vinadaiwa kusikika hadi nje ya ukumbi huo na hivyo kushuhudiwa na baadhi ya watu, akiwemo mwandishi wa habari hii.
Kutokana na hali hiyo, Bogomba alilazimika kuahirisha kikao na wafuasi hao kutoka nje huku wakijifuta machozi na kuondoka katika maeneo hayo ya ofisi hiyo.
Hata hivyo, Kangoye alisema kikao alichoshiriki hakikuwa cha kamati ya siasa, bali kiliitishwa na uongozi wa CCM wilaya ya Tarime ili kuyarejesha pamoja makundi yaliyoshiriki kura za maoni. Kwa mujibu wa Kangoye, kikao hicho kilivunjwa kwa sababu ya kutokuwepo mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM kutoka mkoa wa Mara, Vedastus Mathayo Manyinyi aliyetarajiwa kuwa mmoja wa wajumbe muhimu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment