Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia jambo ambalo nilimbishia karibu mishipa ya fahamu initoke.Aliniambia kwamba vuguvugu lililopo nchini la vijana na hususani wasanii wa muziki wa kizazi kipya kujiunga na vyama vya siasa, linaongozwa na utashi wa kishabiki shabiki tu na pia tamaa ya fedha na kujiongezea tu umaarufu fulani katika jamii
Leo hii,jioni hii,mwanamuziki Nakaaya Sumari,ambaye miezi kadhaa iliyopita alijiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na kukabidhiwa kadi ya uanachama nambari 0227706, amekikacha chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM). Kwa mujibu wa Global Publishers, tendo hilo limefanyika jioni mbele ya mgombea uraisi kwa tiketi ya CCM, Jakaya Mrisho Kikwete huko katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Ni haki yake kufanya hivyo.Hiyo ndio raha na karaha ya demokrasia.Pamoja na hayo,najiuliza,hivi hawa wasanii wanaelewa kweli nguvu waliyonayo katika kujenga au kushawishi fikra za wananchi?Kwa mfano najiuliza,nini kilimsukuma Nakaaya kujiunga na CHADEMA miezi michache tu iliyopita na leo hii kuamua kujiunga na CCM? Je sababu alizozitoa katika uamuzi wake wa kujiunga na CHADEMA miezi michache tu iliyopita zimekwenda wapi?
Nini kinawasukuma vijana wasanii katika siasa?Ni kweli wanakerwa na matatizo yanayowakabili wananchi au nchi kwa ujumla au kuna lingine kama yale aliyonitajia rafiki yangu hapo juu?
Msikilize Nakaaya katika kibao chake kilichompa umaarufu cha Mr.Politician hapo chini.Pengine kuna haja ya kuwa na version ya Ms.Politician pia.
No comments:
Post a Comment