KARIBUNI MCHICHANI

Kwa Habari moto moto Kuhusu Siasa , Uchumi, Maisha, Elimu Na Mengine Mengi.



Friday, August 27, 2010

SAFARI YA MH . DK .KIKWETE KUTOKA MWANAKIJIJI WA LUGOBA HADI IKULU KWA KISHINDO


                                                                                            MH  .J.  KIKWETE

WASIFU



Utangulizi


Mwaka 2010 unafanyika Uchaguzi Mkuu wa Serikali ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atachaguliwa kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano 2010 – 2015. Kwa mujibu wa ratiba



iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, uteuzi wa wagombea Urais utafanyika tarehe 19 Agosti, 2010 na tarehe ya kupiga kura itakuwa tarehe 31 Oktoba, 2010.



Kwa mujibu wa ratiba ya Chama Cha Mapinduzi, wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitakiwa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya Rais, kwa Katibu



Mkuu wa CCM, tarehe 21 Juni, 2010 na mwisho wa kurejesha fomu hizo ilikuwa tarehe 1 Julai, 2010 saa 10:00 jioni. Mwanachama wa CCM pekee aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.



Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, Toleo la Februari, 2010, Kanuni ya 17 fasili ya (viii) (1), inamtaka mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhaminiwa na jumla ya wanachama wa CCM wasiopungua 250 kila mkoa katika mikoa isiyopungua 10 ya Tanzania, mikoa minane ikiwa ni ya Bara na miwili ya Zanzibar.



Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete aliwasilisha fomu zake kwa Katibu Mkuu wa CCM tarehe 1/7/2010 akiwa amedhaminiwa na Wana-CCM 14,069 katika mikoa yote 26. Kanuni zilimtaka adhaminiwe na wanachama 2,500, lakini kutokana na mapenzi makubwa na mapenzi ya wanachama wa CCM ilimlazimu kupita mikoa yote 26 ya Tanzania ambapo pia walikuwepo wanachama wengi ambao walitaka wamdhamini, lakini hawakupata nafasi hiyo.



Kamati Kuu na Halmashauri Kuu zimeridhika kwamba Ndugu Kikwete anazo sifa za kuendelea kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


WASIFU WA NDUGU JAKAYA MRISHO KIKWETE




Kuzaliwa, Elimu na Mafunzo Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950 katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani. Ni mtoto wa sita katika familia ya watoto tisa. Wazazi wake ni Halfani Mrisho Kikwete (Baba) na Asha Kayaka (Mama) ambao wote wametangulia mbele ya haki. Alipata elimu ya msingi (darasa la kwanza hadi la nne) mwaka 1958-1961 katika Shule ya Msingi Lugoba na katika Shule ya Kati ya Lugoba (darasa la tano hadi la nane) mwaka 1962-1965. Mwaka 1966-1969 alisoma Shule ya Sekondari ya Kibaha, kidato cha kwanza mpaka cha nne, na mwaka 1971-1972 alisoma kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari ya Tanga. Mwaka 1972-1975 alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alihitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi. Alipata mafunzo ya Uofisa wa Jeshi katika Chuo cha Uongozi wa Jeshi Monduli, mwaka 1976-1977 na kupata Kamisheni ya kuwa Luteni. Baadaye mwaka 1983 – 1984 alipata mafunzo ya Ukamanda wa Kombania katika chuo hicho hicho.




Haiba katika Uongozi

Kipaji cha uongozi cha Ndugu Kikwete kilianza kujitokeza mapema katika maisha yake. Kuanzia Shule ya Kati, Sekondari hadi Chuo Kikuu alikuwa kiongozi wa wanafunzi. Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Kibaha na baadaye Naibu Kiranja Mkuu wa Wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Tanga.



Katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa mwanaharakati wa siasa za wanafunzi ambapo hatimaye alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu hicho, upande wa Mlimani mwaka 1973/74. Katika nafasi yake hiyo, alikuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanafunzi na kuchochea vuguvugu la kuunga harakati za ukombozi na kupinga sera za kibaguzi za Makaburu, miongoni mwa wanafunzi na jumuiya nzima ya Chuo Kikuu.




Ndani ya Chama, kipaji chake cha uongozi kilichoambatana na moyo wa kujitolea kilijidhihirisha mapema tangu akiwa shuleni. Alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League) katika Shule ya Sekondari ya Kibaha na Shule ya Sekondari ya Tanga. Aidha, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Vijana wa TANU wa Wilaya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1978 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Taifa ya Umoja wa Vijana wa CCM.




Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu mwaka 1975, aliamua kujiunga na utumishi wa Chama, akiacha uwezekano wa maslahi makubwa zaidi Serikalini au kwenye mashirika ya umma. Alianza kazi akiwa Katibu Msaidizi wa Mkoa wa Singida na kupandishwa cheo hadi kuwa Katibu Mtendaji wa Mkoa.



Kote alikopangiwa kazi, alitekeleza majukumu yake kwa ufanisi na uadilifu mkubwa. Alifanya kazi kwa kujituma. Alijidhihirisha kuwa kiongozi mshirikishaji na mwenye kujenga mahusiano mazuri na viongozi wake na wale aliowaongoza. Kwa sababu hiyo kila alipofanya kazi alipata marafiki wengi ndani na nje ya Chama.



Kama kiongozi na mtendaji wa Chama cha TANU na baadaye Chama cha Mapinduzi, Ndugu Kikwete siku zote amekuwa mwaminifu kwa Chama chake, amekuwa tayari kufanya kazi mahali popote, na wakati wowote anapotumwa na Chama chake. Katika kila nafasi ya uongozi wa Chama aliyoshika, Ndugu Kikwete amekuwa mbunifu na mahiri katika kukiongezea Chama umaarufu pamoja na wanachama, wapenzi na mashabiki wake.



Ndugu Kikwete ni mwanamichezo na mtu mwenye haiba na mvuto mkubwa na ana maono ya mbali katika uongozi. Siku zote, tangu anaanza uongozi akiwa shuleni hadi leo hii ambapo ni Rais wa nchi yetu, Ndugu Kikwete amekuwa kiongozi mwadilifu, msikivu, anayejituma na anayewapenda watu wake anaowaongoza.



Uongozi Ndani ya Chama na Umma

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais mwaka 2005, Ndugu Kikwete alikuwa katika utumishi wa Chama na umma kwa miaka 30 na katika muda huo amewahi kuwa Naibu Waziri kwa miaka 2 na Waziri kwa miaka 15. Katika nafasi zote za uongozi wa umma ambazo amewahi kuzitumikia katika kipindi chote hiki, Ndugu Kikwete, amekuwa mchapakazi, mbunifu, na kiongozi makini jambo ambalo lilifanya aendelee kuaminiwa kwa dhamana kubwa zaidi hadi hii ya uongozi wa Taifa letu.



Kwa muhtasari, historia ya uongozi na utumishi wa Chama na umma ya Ndugu Kikwete ni kama ifuatavyo:-Alianza utumishi wa Chama akiwa Katibu Msaidizi wa TANU wa Mkoa, mwaka 1975-1977. Ilipozaliwa CCM, Ndugu Kikwete alikuwa Afisa wa Chama wa kwanza kutoka Tanzania Bara kuhamishiwa Zanzibar na kufanya kazi ya Katibu Msaidizi na Mkuu wa Utawala wa Afisi Kuu ya CCM, Zanzibar, mwaka 1977-1980. Mwaka 1980 alihamishiwa ofisi ndogo ya CCM Makao Makuu, Dar es Salaam akiwa Mkuu wa Utawala na Mkuu wa Idara ya Ulinzi na Usalama. Mwaka 1981 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa CCM, Mkoa wa Tabora alipokaa mpaka mwaka 1983 aliporudishwa Jeshini na kuwa Kamisaa na Mkufunzi Mkuu wa Siasa katika Chuo cha Uongozi wa Jeshi, Monduli. Mwaka 1986 aliteuliwa kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea na baadaye mwaka 1988 alihamishiwa Wilaya ya Masasi.



Novemba 7, 1988, Ndugu Kikwete aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati, na Madini na mwezi Machi 1990 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi 1994. Desemba, 1994 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha mpaka Desemba, 1995 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuwa mtu wa kwanza kushika nafasi hiyo kwa miaka 10 mfululizo mpaka mwaka 2005. Mwaka 1990, Ndugu Kikwete alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo mpaka mwaka 1995. Jimbo hilo lilipogawanywa na kuwa majimbo mawili, akachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo jipya la Chalinze. Alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa miaka 10 hadi mwaka 2005.



Katika uongozi wake Serikalini, Ndugu Kikwete alisimamia vizuri sekta muhimu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu kama vile Maji, Nishati, Madini, Fedha na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Katika kusimamia sekta hizi muhimu, Ndugu Kikwete alikuwa mbunifu, mchapakazi, na mfuatiliaji mahiri, na kwa ajili hiyo alitoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Alipokuwa Wizara ya Maji, Nishati na Madini alianzisha mfumo wa Leseni za ununuzi wa madini uliosaidia kuokoa madini yetu mengi yaliyokuwa yanauzwa kwa njia ya magendo. Katika Wizara ya Fedha, aliimarisha mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali kwa kuanzisha mchakato wa kuunda Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA). Aidha, alianzisha mfumo mpya wa kusimamia mapato ya Serikali na kurejesha imani ya wahisani waliokuwa wamesusia kuipatia misaada Tanzania. Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikuwa muasisi wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.



URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Alipokuwa mgombea mwaka 2005, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza kampeni ya Chama Cha Mapinduzi kishujaa na kwa umahiri mkubwa. Alifika karibu wilaya zote za nchi yetu isipokuwa tatu akitumia usafiri wa gari barabarani. Alitembea zaidi ya kilomita 31,000 akiinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pamoja na wagombea wa CCM wa Udiwani na Ubunge. Kutokana na kazi nzuri za kuinadi Ilani na Sera za Chama Cha Mapinduzi, Chama chetu kilipata ushindi mkubwa kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa asilimia 80.28 ya kura, viti vya Ubunge 206 kati ya 232, sawa na asilimia 88.79, na viti vya Udiwani asilimia 91.46.



Chini ya uongozi wake, Serikali imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa mafanikio makubwa. Takriban asilimia 80 ya malengo na shabaha za Ilani zimetekelezwa na mengine yanaendelea kutekelezwa. Tumefanikiwa hivyo kwa sababu Ndugu Kikwete alihakikisha kwamba bajeti na mipango ya Serikali ya kila mwaka inazingatia malengo ya Ilani ambayo tulimkabidhi mwaka 2005.



Kutokana na kazi nzuri aliyoifanya, Chama Cha Mapinduzi kilipata ushindi mnono wa asilimia 91.7 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2009.



Katika miaka mitano iliyopita, Ndugu Kikwete ameifanya kazi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa bidii kubwa, kwa uadilifu mkubwa, kwa busara kubwa na umakini mkubwa. Katika mazingira ambayo nchi yetu imepitia, kisiasa na kijamii, katika miaka mitano iliyopita, hekima na busara za Kikwete vimewezesha amani, umoja, utulivu na mshikamano wa Taifa letu kuendelea kudumu na kuimarika. Ameendelea kuwa karibu na makundi yote ya watu wa Tanzania na amekuwa msikivu na mvumilivu. Ameendesha nchi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na demokrasia ikashamiri nchini. Ameweka misingi imara ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu katika jamii. Amekuwa anajituma kwa kiasi kikubwa na kusafiri nchi nzima kuwafuata wananchi wake huko waliko na kuwasikiliza shida zao na kuzitatua. Kwa ajili hiyo, ameendelea kuwa kipenzi na tumaini la Watanzania wote.



Katika kipindi chake cha uongozi, kutokana na bidii, ubunifu na ufuatiliaji wake mahiri, Serikali imefanya mambo makubwa ambayo yatabakia katika historia ya nchi yetu kwa kipindi kirefu, ikiwemo ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma, Chuo Kikuu kipya ambacho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 40,000 na kitakuwa moja ya vyuo vikuu vikubwa kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa ujumla, katika kila sekta muhimu kuna program maalum inayoendelea kutekelezwa.



Mwaka 2006 na 2007, Mkutano Mkuu ulimchagua Ndugu Kikwete kuwa Mwenyekiti wa CCM, nafasi ambayo bado anaishikilia hadi sasa. Chini ya uongozi wake, CCM imeweza kuimarika kwa kuongeza wanachama, wapenzi na mashabiki. Lakini pia Ndugu Kikwete amefanya kazi kubwa ya kuimarisha safu za watendaji wa Chama Mikoani na Wilayani na kuwapatia vitendea kazi muhimu na kuboresha maslahi.



Ndugu Kikwete amekuwa kiongozi wa kuaminiwa, kutumainiwa na kutegemewa kwa ushauri, mawazo na uongozi katika masuala mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa. Kwa ajili hiyo, amekuwa anahusishwa katika mikutano na masuala mbalimbali ya kimataifa na kikanda. Kutokana na jitihada zake na uwezo wake mkubwa katika medani ya diplomasia, nchi yetu imepata sifa na heshima kubwa na imeendelea kuaminiwa kimataifa. Katika kipindi cha Urais wake, Ndugu Kikwete amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na mshiriki na kiongozi wa kutumainiwa katika masuala mbalimbali yanayohusu usalama na maendeleo duniani.



Katika kuutambua uwezo wa Ndugu Kikwete na kuuthamini mchango wake katika kuendeleza ustawi wa jamii, demokrasia na uchumi, vyuo vikuu kadhaa vyenye majina makubwa duniani vimemtunuku Shahada za Heshima za Udaktari wa Falsafa.



PENDEKEZO LA HALMASHAURI KUU YA TAIFA

Kutokana na sifa hizo mahsusi za Ndugu Kikwete, na mafanikio makubwa ambayo Taifa letu limeyapata katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, na kutokana na haja ya kuyaendeleza na kuyadumisha mafanikio haya, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imempitisha Ndugu Kikwete kuwa Mgombea pekee wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM. Halmashauri Kuu ya Taifa inayo heshima na fahari kubwa kuwasilisha mbele ya Mkutano huu Mkuu Maalum wa Taifa wa CCM, na kuwaomba Wajumbe wote wampigie kura zote za Ndiyo ili awe mgombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010.




 
 
MUNGU IBARIKI TANZANIA , MUNGU UBARIKI UCHAGUZI 2010

No comments:

Post a Comment